Friday, 8 October 2010

saratani ya ngozi kwa albino ni janga la taifa

http://www.mwananchi.co.tz/makala/-/5357-saada-saratani-inakula-uso-wangu

Na Florence Majani.gazeti Mwananchi Oct 7, 2010

MSISIMKO wa ajabu lazima ukukumbe pale utakapokutana naye akiwa na kidonda kilichosababisha shimo katika mwamba wa pua yake.  Huku juu ya shavu lake la kulia kuna kovu la kidonda nacho kikiwa kimetengeneza shimo na kuufanya uso wake uwe wa kustaajabisha.
Saada Rashid amezaliwa  Ifakara, Morogoro, miaka 30 iliyopita akiwa ni binti  pekee kwa wazazi wake. Amezaliwa na  ulemavu wa ngozi huku akitoka katika familia yenye kipato duni, hivyo  maisha yake kuwa ya kubahatisha kila kunapokucha.
Anasema, kwa bahati mbaya mama yake alifariki mwaka 2005, na kwa sababu asingeweza kuishi kwa mama wa kambo ilimbidi akaishi kwa shangazi yake na huko hali haikuwa shwari.

“Shangazi yangu naye hakuwa na maisha mazuri, tulikuwa na maisha ya tabu, baya zaidi mjomba wangu alikuwa hanitaki na alipenda   kulalamika sana. Maneno yake ya chinichini yalizidi baada ya mimi kupata ujauzito. Mjomba alidiriki kumtamkia shangazi kuwa hanitaki kama nisingeondoka basi angemfukuza hata na shangazi,”anasema Saada
Kwa bahati mbaya Saada alipachikwa ujauzito huo na mume wa mtu, ambaye mbali na kuwa na watoto, pia hana shughuli yoyote ya kumuingizia kipato.

Maisha ya Saada yalikuwa hatarini na hakuwa na muelekeo baada ya shangazi yake kuitii amri ya mjomba wake na kumfukuza.
“Nilipojifungua tu ndipo nilipofukuzwa rasmi nyumbani kwa shangazi yangu, nikaamua kujitafutia mahali pa kuishi, sikuwa na ndugu yoyote, nikachukua uamuzi wa kwenda katika nyumba ya masista, kituo cha masista cha kulea watu wenye ukoma. Nikaomba wanipe msaada mimi na mwanangu kwa bahati nzuri nilimkuta sista mmoja, Maria Paulo huyo alinionea huruma na akanisaidia nikaanza rasmi kuishi katika kituo hicho,” anasema  Saada.

Hakupenda kuishi katika kituo kile, alitamani ajitegemee na  amlee mtoto wake wa kike aliyempa jina la Swaiba. Akamuomba sista Maria ampe fedha za kujikimu akaanze maisha kijijini kwao Ifakara.
“Nikamuomba sista Maria anipe msaada ili nikatafute kiwanja nianze maisha ya kujitegemea, akaniambia anao uwezo wa kunipa shilingi laki nne tu na akasema hana fedha zaidi ya hizo. Nikasaidiwa kupata kiasi hicho cha fedha  nikaenda kijijini kwetu nikanunua kiwanja kwa shilingi 70,000, na kisha nikajenga nyumba ya matofali ya kuchoma, nikawa nalima napata chakula kidogo,”anasema.

Baada ya muda akaanza kuona kidonda kidogo katika paji lake la uso, akaenda hospitali  ya Ifakara akatibiwa kwa kutiwa dawa na  kufungwa lakini kidonda kile hakikupona kabisa na ndipo alipopewa barua ya kwenda hospitali ya taifa ya  Muhimbili.
“Pale Muhimbili nikafanyiwa vipimo  madaktari wakasema haikuwa kansa ni vidonda vya kawaida nikapewa dawa za kunywa na kupaka nikarudi Ifakara lakini kidonda kile hakikupata nafuu yoyote nikaenda  tena Muhimbili.
Safari hii nikakwanguliwa nyama ya paji la uso pale kwenye kidonda halafu wakanikata nyama katika paja langu la kulia na kuziba shimo la kwenye  uso,”anaelezea Saada.
Hata hivyo amani ya Saada haikudumu kwa muda mrefu kwani   October 2008, kikaanza kidonda kipya, safari hii kikiwa juu kidogo ya sikio. Hata hivyo hakuweza kufanya lolote kwa sababu hakuwa na fedha hata za kula yeye na mtoto wake na kipindi hicho alikuwa amebeba  ujauzito wa pili.

“Nikashindwa kwenda hospitali sikuwa na fedha kabisa, nikaamua kwenda kwa shangazi yangu kumuomba msaada kwani kidonda kilikuwa kinaniuma na sikuwa nikilala usiku isitoshe nilikuwa nina ujauzito wa mtoto huyu. Watoto wa shangazi wakachanga shilingi elfu tano tano kila mmoja wakanipa niende hospitali,”anaeleza.
Kile alichokitegemea hospitali ya Ifakara sicho alichokipata, kwani baada ya madaktari kumpima wakashauri akatwe sehemu ya nyama yake ili ikapimwe Ulaya na hapo alitakiwa atoe shilingi 30,000.

“Sikuwa na fedha hizo ndipo wakaniambia niende Ocean Road, wakaniambia nisubiri barua, niliisubiri kwa miezi mitatu hadi Desemba 2009 ndipo nilipopewa na   kuipeleka Ocean Road, sikuwa na nauli.  Nikaamua kumtafuta yule sista Maria aliyenisaidia kipindi kile nikaenda katika kituo alichokuwa akikaa kwa bahati mbaya nikaambiwa mtu huyo alikwisharudi Ulaya. Nilikosa nguvu nikakata tamaa, nikajikaza na kuwaelezea matatizo yangu  nikawaambia sipajui Dar es Salaam wala sina ndugu  wakanipa 20,000,”anasema Saada.

Nauli ya kutoka Ifakara kwenda Dar es Salaam, ilikuwa ni shilingi 20,000 hivyo mkononi mwake alikuwa na kiasi hicho tu bila akiba ya matumizi mengine akiwa na mtoto mdogo wa miezi mitano mgongoni mwake.
“Ikanibidi nitafute mtu wa kumuachia mtoto yaani Swahiba nikamuacha kwa shangazi yangu. Kwa bahati nzuri nikiwa katika gari nikakutana na msamaria mwema, mama Shukuru ambaye alinipa msaada mkubwa. Nilipofika hapa Dar   es Salaam nikafikia nyumbani kwake Yombo. Asubuhi siku iliyofuata akanileta hapa Ocean Road,”anasimulia Saada.

Alipofika Ocean Road madaktari wa pale walimwambia aende Muhimbili akachukue  kwanza vipimo  ili wavifanyie kazi. Hatua za uchukuaji wa vipimo hivyo haukuwa wa siku moja na ilimbidi apewe kitanda  lakini hilo halikuwezekana.
“Muhimbili walikataa mimi kulazwa nikiwa na mtoto wa miezi mitano, ikanibidi nikae kwa mama Shukuru huku nikiendelea kufanya  vipimo nikawa nasaidiwa nauli na jirani mwingine kwa sababu hata mwenyeji wangu hakuwa na uwezo wa kunipa nauli ya kila siku,” anasema Saada.

Anasema, machi 23 mwaka huu akafanikiwa kupelekwa Ocean Road akagundulika kuwa saratani inamla sehemu za usoni na kwenye ubongo. Ndipo madaktari wakaamua aanzishiwe tiba ya mionzi.
“Nikaanza na tiba ya mionzi, nikapigwa mionzi 10 mara ya kwanza na mara ya pili nikapigwa mionzi saba nikaruhusiwa na  kuambiwa nirudi tena  Septemba 15,”anaeleza.

Kabla ya tarehe ya kurudi kiliniki kikaanza kidonda cha puani, kila alipoenda kukitibu hospitali hakikupona, ndipo alipoamua kutafuta nauli na alipopata alipanda treni na kuja Dar es Salaam.
“Nilifikia tena kwa mama Shukuru, nikapewa kitanda hapa Ocean Road nikaanza matibabu nikakatwa tena nyama hapa puani na nikaendelea na tiba ya mionzi,”anasema.

Pamoja na kuugulia maumivu makali yasababishwayo na saratani  inayomla katika uso wake, inambidi Saada akae na mtoto wake  mdogo mwenye mwaka mmoja hospitalini hapo.  Uso wake unaendelea kumegwa siku hadi siku kwa sababu kansa hiyo ipo mwilini mwake, hana msaada wa kifedha kwake na mtoto wake.

Kwa huzuni huku machozi  yakimtoka Saada anasema, “Sikupenda kuwa hivi, napata mateso makali sana. Natamani kupona, natamani kufanya kazi lakini sijasoma nimekomea darasa la nne hata hivyo naweza kufanya kitu cha kuniingizia fedha kwa kukodi shamba na kutafuta  vibarua watakaolima, kwa sababu nimeambiwa nisikae juani”.

Leo ni Saada na kesho ni wewe, mzazi wako au  ndugu yako haya humkuta kila mtu mwenye pumzi bila kupanga wala kupenda. Maisha yake ni ya taabu anahitaji msaada wako kwani hakupenda kuwa mlemavu na wala hakuombea saratani hii imtafune usoni.
Kwa yeyote ambaye anapenda kumsaidia anaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala haya 0715773366

No comments:

Post a Comment