Tuesday, 3 July 2012

AKINAMAMA WAZEE KWELI WANASTAHILI UKATILI HUU?




 AKINAMAMA WAZEE KWELI WANASTAHILI UKATILI HUU?
Mpendwa msomaji hebu jenga kwanza taswira hii kichwani mwako:
“Ni saa moja kamili jioni katika kijiji hiki kidogo wilayani Misungwi mkoani Mwanza. Mwanamke mzee wa takribani  miaka 75, anaonekana akiingiza kuni katika kibanda kidogo pembeni ya nyumba yake chakavu. Kibanda hiki kidogo cha udongo kimekuwepo kwa miaka miaka mingi na humo siku hadi siku, chakula cha asubuhi, mchana na usiku hupikwa na kuendeleza maisha ya bibi huyu. Mbali ya kuni pia hutumia mavi ya ngo’mbe makavu kutengeneza moto wa kupikia.

Bibi huyu mpweke ni mjane. Huku akichochea moto jikoni tayari kupika uji, ghafla anajiunguza kidole na kukunja uso wake kwa maumivu makali. Ndipo anapogundua mawazo yake hayapo katika kile anachokifanya muda huo. Anarudi nyuma kidogo na kukaa juu ya kigoda kidogo. Uso wake unaonesha hofu ya dhahiri.

Bibi anakumbuka namna mmoja wa majirani zake alivyomwijia saa moja iliyopita na kumweleza habari za kushtua sana. Katika maisha yake bibi huyu hajawahi kutishika kama ilivyotokea wakati ule akipewa habari zile. Jirani yule alimsihi bibi atafute namna yoyote ya kukimbia toka kijijini pale ili kulinda maisha yake dhidi ya jirani kadhaa wanaofikiria kumuangamiza. Jirani yule hakutaka kuongea sana alihitimisha maongezi yake na kuondoka kwa uficho kama vile alivyokuja akimwacha bibi huyu katika kitisho kikubwa.

Akiwa pale jikoni jioni hii huku giza likianza kutanda, wasiwasi unazidi kuvamia mawazo ya bibi. Anawaza ni kitu gani kinaweza kuwa kimewatuma baadhi ya watu wafikirie kumwangamiza wakimtuhumu kuwa mchawi.

Anawaza katika maisha yake hakuwahi kujishughulisha na kitu chochote kinachoitwa uchawi. Katika maisha yake ya ujana yeye na marehemu mume wake mzee Nyanda waliwahi kushuhudia vitendo vingi vya ukamataji na mauaji ya akina mama wazee kwa tuhuma za uchawi. Lakini hakuwahi kuwaza hata kidogo kwamba siku moja na yeye anaweza kujikuta katika hofu ya kuuawa kwa panga na shoka kama alivyofanyiwa bibi mmoja kijijini hapa miezi miwili iliyopita! 

HOFU kubwa inamshika bibi huyu na anajiinua kwa uchovu na kutoka nje kuelekea katika nyumba yake iliyo pembeni kidogo ya jiko. Anapoingia chumbani kwake anakwenda moja kwa moja mezani na kuchukua kioo alichonunua hivi karibuni katika mnada na kujitazama usoni. Siku zote anajua ya kuwa macho yake ni mekundu. Ila leo wekundu huu anauona ni mkubwa mno. HOFU kubwa sasa inatambaa katika kila kona ya mwili wake ambao katika kipindi cha miaka miwili umekuwa dhaifu kutokana na maradhi ya kifua. Anawaza jambo moja tu! Wapi akajifiche kabla usiku haujawa mwingi kisha asubuhi atafute namna ya kwenda mjini kwa mjukuu wake. Anawaza kwenda kujificha katika shamba lake lakini anajua hataweza kuikabili baridi na hali yake ya maradhi ya kifua. Machozi yanamlenga lenga bibi Nyanda. HOFU kubwa inazidi kutambaa vilivyo ndani ya mwili wake mnyonge.

Hiyo ni taswira ambayo iliwahi kunipitia katika mawazo yangu miaka ya nyuma baada ya  kusoma katika gazeti habari ya bibi mmoja aliyeuawa kikatili wilayani Misungwi kwa tuhuma za uchawi. Habari ile haikueleza kwa undani mauaji yale yalivyotokea, lakini iliniacha na maswali mengi. Lakini toka miaka hiyo ya themanini mwishoni nikiwa shule ya msingi hadi leo hii katika utuuzima wangu kila mwaka na kila mwezi nimeendelea kusoma magazetini na kusikia radioni habari za kuuawa watu kwa tuhuma za uchawi. Wahanga wa mambo hayo hasa akina mama wazee huvamiwa na kukatwa mapanga hadi kufa.

Jambo moja la kusikitisha ni kwamba mauaji haya yanatokea wakati sheria inayohusu mambo ya uchawi ipo. Sheria hii ingeweza kutumika vyema kusimamia mashtaka kama kuna watu wanatuhumiwa kujihusisha na uchawi badala ya watu fulani kuamua tu kirahisi kuchukua sheria mikononi mwao na kuwahukumu wengine kikatili kabisa na kukatisha maisha yao huku serikali na vyombo vyake vya utawala ikiyajua haya kwa miaka lukuki! Huu ni ukatili mkubwa sana.

Sheria hii (The Tanzania Witchcraft Act, Cap.18) inatoa maana ya uchawi kuwa ni vitendo vya ulozi au uchawi, kuroga na matumizi ya vifaa vinavyohusiana na uchawi pamoja na kuwa na maarifa yanayohusiana na nguvu za giza (occult knowledge). Kifungu cha 131 cha sheria ya uchawi kinaeleza adhabu stahili za makosa haya pamoja na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu pale inapotokea mauaji yametendeka. Sasa kwanini taratibu hizi hazitumiki na tumeacha ukatili huu mkubwa dhidi ya akina mama hawa kuendelea kwa miaka mingi kiasi hiki?

Jambo jingine la kuhuzunisha ni kwamba bado janga hili liko sana mikoa ile ile ya Mwanza na Shinyanga. Kama ambavyo hali ilivyokuwa miaka ya sabini bado pia hali iko hivyo hivyo miaka hii. Ungetegemea kwamba hii ingekuwa ni nafuu katika jitihada za kulitokomeza tatizo kwa kuwekeza nguvu katika mikoa hiyo na kuubeba uzoefu na kuupeleka sehemu nyingine za nchi zenye ukatili huu.

Wakati nikiipitia ripoti ya haki za binadamu Tanzania ya mwaka 2011 iliyotolewa hivi karibuni na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, niliona kwamba kati ya mwaka 2005 na 2011, takribani watu 3,000 waliuawa kiholela (lynching) na majirani zao kwa tuhuma za uchawi. Kitakwimu, hii ni sawa na watu 500, hasa hasa wanawake wazee wenye macho mekundu kuuawa kila mwaka nchini Tanzania!  Ripoti hii inalinukuu gazeti moja la Nipashe la mwezi wa nane mwaka 2011 likiandika watu 242 waliuawa kwa tuhuma hizo kuanzia mwezi wa kwanza 2010 hadi mwezi wa sita 2011. Taarifa ya polisi nayo iliyonukuliwa katika ripoti hii inaonesha ukuaji wa tatizo hili ambapo mwaka 2010 watu 579 waliuawa ukilinganisha na watu 642 waliouwa mwaka 2011.

Alama kubwa inayowaweka akinamama wazee katika hatari ya kuuawa kwa imani za kishirikina hasa katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga ni kuwa na macho mekundu. Watu wanaofuatilia mambo haya tunajua kuwa wekundu huu unasababishwa na matumizi ya kinyesi cha ng’ombe na aina fulani ya miti ya kuni kwa muda mrefu katika shughuli za upishi. Ule moshi unaofuka unawaacha akina mama hawa katika madhara hayo. Lakini la kujiuliza hapa ni je, wadau wa haki za binadamu ikiwemo serikali na asasi za kiraia tumeshindwa kabisa kupiga kampeni nzito ya uelimishaji juu ya suala hili? Au tuseme kwamba kwa kuwa sehemu kubwa ya watanzania tunaamini katika uwepo wa uchawi na mambo yanayohusiana nao basi imetufanya tusione uzito wa tatizo hili? Inawezekana tunafikiri kwamba ni stahili yao akinamama hawa kuuawa kwa kuwa ni wachawi. Eeeh Mungu!
Jitihada za kutafuta ufumbuzi wa mauaji haya lazima ziangalie ufahamu wa jamii za kisukuma na nyingine nchini katika kushughulikia matatizo yao ya kila siku. 

Kitendo cha jirani kukumbwa na masaibu, iwe ni maradhi ya mwanae, mavuno hafifu, kufiwa, na mengine, kisha akawa mwepesi kuhitimisha kuwa lazima yule bibi mwenye macho mekundu ndiye mlozi anayekwaza maisha yake, tunajifunza mengi.
Kitendo cha mvuvi au mfanyabiashara wa madini kwenda kwa mganga ili apewe dawa ya kusaidia kuongeza mafanikio katika biashara, tunajifunza mengi.

Kitendo cha mtu kukubali kupeleka viungo vya albino kwa mganga ili kutengeneza dawa ya utajiri, tunajifunza mengi. 

Tuingie ndani kabisa ya falsafa na imani za watu hawa na kupiga kampeni kubwa ya kitaifa itakayofanikiwa na kukomesha milele mauaji haya ambayo mimi nadiriki kuyaita ukatili mkubwa dhidi ya ubinadamu. Ni aibu na fedheha kubwa kwamba ndani ya Tanzania hii kuna watu wanawindwa na kuuliwa kama wanyama! Ni uvunjaji mkubwa wa katiba kwa sababu ile hifadhi ya maisha na usalama anaostahili kila binadamu ndani ya Tanzania yetu imeondolewa dhidi ya akina mama hawa wa kisukuma wa Shinyanga na Mwanza. Lakini bado tunajivuna kwamba watu wetu wanaishi kwa amani na utulivu! Hii ni kejeli kubwa sana.

Nahitimisha kwamba, katika utafiti mmoja uliowahi kufanywa na Tume ya Haki za Binadamu, iligundulika pia kuwa tuhuma za uchawi wakati mwingine ni kisingizio tu. Mwanamke mjane anasingiziwa kuwa ni mlozi na anauawa lakini kumbe wauaji malengo yao ni kunyakua mashamba na mali zingine za marehemu. Hiyo inaweza kutekelezwa na ndugu wa mume wa mwanamke yule ili kuondoa vikwazo katika azma yao ya kujipatia utajiri. Hizi sababu nazo ziangaliwe sana.

Chonde chonde tukomeshe mauaji haya sasa! 

Moses Gasana
Mawazo Chanya Media
0713-480670
mosesgasana@yahoo.com