AKINAMAMA WAZEE KWELI WANASTAHILI UKATILI HUU?
Mpendwa msomaji hebu jenga kwanza taswira hii
kichwani mwako:
“Ni saa moja
kamili jioni katika kijiji hiki kidogo wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Mwanamke mzee wa takribani miaka
75, anaonekana akiingiza kuni katika kibanda kidogo pembeni ya nyumba yake
chakavu. Kibanda hiki kidogo cha udongo kimekuwepo kwa miaka miaka mingi na
humo siku hadi siku, chakula cha asubuhi, mchana na usiku hupikwa na kuendeleza
maisha ya bibi huyu. Mbali ya kuni pia hutumia mavi ya ngo’mbe makavu
kutengeneza moto wa kupikia.
Bibi huyu
mpweke ni mjane. Huku akichochea moto jikoni tayari kupika uji, ghafla
anajiunguza kidole na kukunja uso wake kwa maumivu makali. Ndipo anapogundua
mawazo yake hayapo katika kile anachokifanya muda huo. Anarudi nyuma kidogo na
kukaa juu ya kigoda kidogo. Uso wake unaonesha hofu ya dhahiri.
Bibi
anakumbuka namna mmoja wa majirani zake alivyomwijia saa moja iliyopita na
kumweleza habari za kushtua sana. Katika maisha yake bibi huyu hajawahi
kutishika kama ilivyotokea wakati ule akipewa habari zile. Jirani yule alimsihi
bibi atafute namna yoyote ya kukimbia toka kijijini pale ili kulinda maisha
yake dhidi ya jirani kadhaa wanaofikiria kumuangamiza. Jirani yule hakutaka
kuongea sana alihitimisha maongezi yake na kuondoka kwa uficho kama vile
alivyokuja akimwacha bibi huyu katika kitisho kikubwa.
Akiwa pale
jikoni jioni hii huku giza likianza kutanda, wasiwasi unazidi kuvamia mawazo ya
bibi. Anawaza ni kitu gani kinaweza kuwa kimewatuma baadhi ya watu wafikirie
kumwangamiza wakimtuhumu kuwa mchawi.
Anawaza katika
maisha yake hakuwahi kujishughulisha na kitu chochote kinachoitwa uchawi.
Katika maisha yake ya ujana yeye na marehemu mume wake mzee Nyanda waliwahi
kushuhudia vitendo vingi vya ukamataji na mauaji ya akina mama wazee kwa tuhuma
za uchawi. Lakini hakuwahi kuwaza hata kidogo kwamba siku moja na yeye anaweza
kujikuta katika hofu ya kuuawa kwa panga na shoka kama alivyofanyiwa bibi mmoja
kijijini hapa miezi miwili iliyopita!
HOFU kubwa
inamshika bibi huyu na anajiinua kwa uchovu na kutoka nje kuelekea katika
nyumba yake iliyo pembeni kidogo ya jiko. Anapoingia chumbani kwake anakwenda
moja kwa moja mezani na kuchukua kioo alichonunua hivi karibuni katika mnada na
kujitazama usoni. Siku zote anajua ya kuwa macho yake ni mekundu. Ila leo
wekundu huu anauona ni mkubwa mno. HOFU kubwa sasa inatambaa katika kila kona
ya mwili wake ambao katika kipindi cha miaka miwili umekuwa dhaifu kutokana na
maradhi ya kifua. Anawaza jambo moja tu! Wapi akajifiche kabla usiku haujawa
mwingi kisha asubuhi atafute namna ya kwenda mjini kwa mjukuu wake. Anawaza
kwenda kujificha katika shamba lake lakini anajua hataweza kuikabili baridi na
hali yake ya maradhi ya kifua. Machozi yanamlenga lenga bibi Nyanda. HOFU kubwa
inazidi kutambaa vilivyo ndani ya mwili wake mnyonge.
Hiyo ni taswira ambayo iliwahi kunipitia katika
mawazo yangu miaka ya nyuma baada ya
kusoma katika gazeti habari ya bibi mmoja aliyeuawa kikatili wilayani
Misungwi kwa tuhuma za uchawi. Habari ile haikueleza kwa undani mauaji yale yalivyotokea,
lakini iliniacha na maswali mengi. Lakini toka miaka hiyo ya themanini mwishoni
nikiwa shule ya msingi hadi leo hii katika utuuzima wangu kila mwaka na kila
mwezi nimeendelea kusoma magazetini na kusikia radioni habari za kuuawa watu
kwa tuhuma za uchawi. Wahanga wa mambo hayo hasa akina mama wazee huvamiwa na
kukatwa mapanga hadi kufa.
Jambo moja la kusikitisha ni kwamba mauaji haya
yanatokea wakati sheria inayohusu mambo ya uchawi ipo. Sheria hii ingeweza
kutumika vyema kusimamia mashtaka kama kuna watu wanatuhumiwa kujihusisha na
uchawi badala ya watu fulani kuamua tu kirahisi kuchukua sheria mikononi mwao
na kuwahukumu wengine kikatili kabisa na kukatisha maisha yao huku serikali na
vyombo vyake vya utawala ikiyajua haya kwa miaka lukuki! Huu ni ukatili mkubwa
sana.
Sheria hii (The
Tanzania Witchcraft Act, Cap.18) inatoa maana ya uchawi kuwa ni vitendo vya
ulozi au uchawi, kuroga na matumizi ya vifaa vinavyohusiana na uchawi pamoja na
kuwa na maarifa yanayohusiana na nguvu za giza (occult knowledge). Kifungu cha 131 cha sheria ya uchawi kinaeleza
adhabu stahili za makosa haya pamoja na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu
pale inapotokea mauaji yametendeka. Sasa kwanini taratibu hizi hazitumiki na
tumeacha ukatili huu mkubwa dhidi ya akina mama hawa kuendelea kwa miaka mingi
kiasi hiki?
Jambo jingine la kuhuzunisha ni kwamba bado janga
hili liko sana mikoa ile ile ya Mwanza na Shinyanga. Kama ambavyo hali
ilivyokuwa miaka ya sabini bado pia hali iko hivyo hivyo miaka hii. Ungetegemea
kwamba hii ingekuwa ni nafuu katika jitihada za kulitokomeza tatizo kwa
kuwekeza nguvu katika mikoa hiyo na kuubeba uzoefu na kuupeleka sehemu nyingine
za nchi zenye ukatili huu.
Wakati nikiipitia ripoti ya haki za binadamu
Tanzania ya mwaka 2011 iliyotolewa hivi karibuni na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu, niliona kwamba kati ya mwaka 2005 na 2011, takribani watu 3,000 waliuawa kiholela (lynching) na majirani
zao kwa tuhuma za uchawi. Kitakwimu, hii ni sawa na watu 500, hasa hasa
wanawake wazee wenye macho mekundu kuuawa kila mwaka nchini Tanzania! Ripoti hii inalinukuu gazeti moja la
Nipashe la mwezi wa nane mwaka 2011 likiandika watu 242 waliuawa kwa tuhuma
hizo kuanzia mwezi wa kwanza 2010 hadi mwezi wa sita 2011. Taarifa ya polisi
nayo iliyonukuliwa katika ripoti hii inaonesha ukuaji wa tatizo hili ambapo
mwaka 2010 watu 579 waliuawa ukilinganisha na watu 642 waliouwa mwaka 2011.
Alama kubwa inayowaweka akinamama wazee katika
hatari ya kuuawa kwa imani za kishirikina hasa katika mikoa ya Mwanza na
Shinyanga ni kuwa na macho mekundu. Watu wanaofuatilia mambo haya tunajua kuwa
wekundu huu unasababishwa na matumizi ya kinyesi cha ng’ombe na aina fulani ya
miti ya kuni kwa muda mrefu katika shughuli za upishi. Ule moshi unaofuka
unawaacha akina mama hawa katika madhara hayo. Lakini la kujiuliza hapa ni je,
wadau wa haki za binadamu ikiwemo serikali na asasi za kiraia tumeshindwa
kabisa kupiga kampeni nzito ya uelimishaji juu ya suala hili? Au tuseme kwamba
kwa kuwa sehemu kubwa ya watanzania tunaamini katika uwepo wa uchawi na mambo
yanayohusiana nao basi imetufanya tusione uzito wa tatizo hili? Inawezekana
tunafikiri kwamba ni stahili yao akinamama hawa kuuawa kwa kuwa ni wachawi.
Eeeh Mungu!
Jitihada za kutafuta ufumbuzi wa mauaji haya lazima
ziangalie ufahamu wa jamii za kisukuma na nyingine nchini katika kushughulikia
matatizo yao ya kila siku.
Kitendo cha jirani kukumbwa na masaibu, iwe ni
maradhi ya mwanae, mavuno hafifu, kufiwa, na mengine, kisha akawa mwepesi
kuhitimisha kuwa lazima yule bibi mwenye macho mekundu ndiye mlozi anayekwaza
maisha yake, tunajifunza mengi.
Kitendo cha mvuvi au mfanyabiashara wa madini kwenda
kwa mganga ili apewe dawa ya kusaidia kuongeza mafanikio katika biashara,
tunajifunza mengi.
Kitendo cha mtu kukubali kupeleka viungo vya albino
kwa mganga ili kutengeneza dawa ya utajiri, tunajifunza mengi.
Tuingie ndani kabisa ya falsafa na imani za watu
hawa na kupiga kampeni kubwa ya kitaifa itakayofanikiwa na kukomesha milele
mauaji haya ambayo mimi nadiriki kuyaita ukatili mkubwa dhidi ya ubinadamu. Ni
aibu na fedheha kubwa kwamba ndani ya Tanzania hii kuna watu wanawindwa na
kuuliwa kama wanyama! Ni uvunjaji mkubwa wa katiba kwa sababu ile hifadhi ya
maisha na usalama anaostahili kila binadamu ndani ya Tanzania yetu imeondolewa
dhidi ya akina mama hawa wa kisukuma wa Shinyanga na Mwanza. Lakini bado
tunajivuna kwamba watu wetu wanaishi kwa amani na utulivu! Hii ni kejeli kubwa
sana.
Nahitimisha kwamba, katika utafiti mmoja uliowahi
kufanywa na Tume ya Haki za Binadamu, iligundulika pia kuwa tuhuma za uchawi
wakati mwingine ni kisingizio tu. Mwanamke mjane anasingiziwa kuwa ni mlozi na
anauawa lakini kumbe wauaji malengo yao ni kunyakua mashamba na mali zingine za
marehemu. Hiyo inaweza kutekelezwa na ndugu wa mume wa mwanamke yule ili
kuondoa vikwazo katika azma yao ya kujipatia utajiri. Hizi sababu nazo
ziangaliwe sana.
Chonde chonde tukomeshe mauaji haya sasa!
Moses Gasana
Mawazo Chanya Media
0713-480670
mosesgasana@yahoo.com
