Marehemu Munga Tehenan, wakati wa uhai wake alikuwa mwandishi mahiri wa habari nchini Tanzania. Baadae akaanzisha gazeti la Jitambue.Lilikuwa likitoka kila Jumatano na makala kuhusu elimu ya utambuzi. Humo ulikuwa ukipata habari za namna ya kujenga haiba yako, kujiamini na kuwa na mawazo chanya yanayoweza kusukuma mbele maisha yako na ukaishi kwa mafaniko na furaha. Munga aliandika sana akiwausia watu kubadilika na kuachana na mawazo ya kulogwa, au kuwa na nuksi katika maisha.
Jamaa hakuchoka.Alikuwa mchapa kazi akisistiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujipatia mafaniko na furaha.Alipiga vita sana mawazo hasi, akiyasema kuwa ndo chanzo cha maradhi na watu kuwa na maisha yaso na furaha wala amani.
Munga hakika nikiwa mmoja wa wasomaji wake niliipenda elimu ile ambayo aliitoa vyema akitumia mifano hai ya maisha ya hapa Tanzania.Nilipata inspiration kubwa sana baada ya kusoma habari hizo kiasi kwamba baada ya kipindi fulani nikawa mmoja wa wachangiaji katika gazeti lile.
Leo hii naweza kusema Munga alitoa mchango mkubwa sana katika kuyabadilisha maisha yangu na kuwa ya furaha. Inspiration niliyopata kutokana na juhudi zake ni kubwa mno.Hakika Yahwe amlaze mahali pema peponi amina.
Hapa chini ni moja ya makala zake kama nilivyoichukua toka blog ya ndugu Shaban Kaluse-http://kaluse.blogspot.com/2008/11/je-hayati-munga-tehenan-aliwahi.html
"Ili kufanikiwa kwenye lengo lolote katika maisha, ni lazima uamini kwamba utafanikiwa. Kama usipofanya hivyo, una nafasi kubwa ya kushindwa.
Unaweza kuwa na malengo mapya uliyoyapanga na ambayo unaanza kujaribu kuyatekeleza. Lakini ni lazima ufanye hivyo ukiwa na imani kubwa kwamba utafanikiwa.
Waweza kuona kazi uliyo nayo hivi sasa haikusaidii sana na hivyo kuamua ghafla kuiacha.Waweza kufanya hivyo huku ukiwa hujaamua kitu gani cha kufanya, na hivyo kulazimika kutumia kipindi cha pengine miezi sita ama hata zaidi inayofuata kujaribu kufikiria nini cha kufanya.
Huwezi kufanikiwa katika kile unachokitaka kufanya ikiwa hutaamua kuyafanya mawazo yako hayo uliyonayo kuwa vitendo. Hata ukiwa na kiu na hamu kubwa kiasi gani ya kufanikiwa, bila kuhamasisha nafsi yako na kuanza kufuatilia lile unalotaka kulifanya, kufanikiwa itakuwa ndoto kwako. Hilo litashusha ari yako na kujikuta unarudi kulekule ulikotoka, kwenye kazi ya kuajiriwa.
Lakini wakati wote huu, vyanzo vya mafanikio huwepo karibu nawe tayari kutumiwa nawe kwa ajili ya kukuletea mafanikio unayoyataka. Lakini bila kuiamini nafsi yako kwamba unaweza kufanikiwa, huwezi kufanikiwa.
Hivyo ni lazima ujifikirie katika mambo unayoyafanya, unafanya mambo yako yanayokuelekeza kwenye malengo yako ukiwa na imani kwamba utafanikiwa. Je, unayo picha ya mafanikio yako akilini mwako na hisia kwamba hivi ndivyo inavyotakiwa kuwa?
Hebu kaa chini na ufikirie kuhusu mambo uliyowahi kuyafanya na ukashindwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita. Jiulize ikiwa kweli ulijiamini kwa dhati kwamba utafanikiwa.
Mara nyingi utakuta katika matukio hayo ulikuwa na mashaka ndani yako kuhusiana na uwezo wako wa kufanikiwa na hivyo iko haja ya kujihamasisha kabla ya kuanza kupiga hatua kuelekea kwenye lengo lako. Unatakiwa kuamini kwamba utafanikiwa.
Ni kwa nini imani hiyo ni muhimu kiasi hicho? Kwa kawaida huwa tunaanza kujenga imani tangu tukiwa wadogo. Mara baada ya kuzaliwa kwetu, huanza kujenga au kujengewa imani.
Na baadaye tunaendelea kujijengea imani wakati tukiendelea kukua na huwa tunabadili imani kutoka za zamani na kujenga mpya, kutegemea vitu vingi. Tunahitaji kufanya haya ili kuyafanya maisha yetu hapa duniani yawe rahisi na ya kweli.
Siku zote tunaamini kwamba tunapoamka vitandani mwetu asubuhi, tunahitajika kuweka miguu yetu chini ili kuweza kusimama ardhini kabla ya kuendelea na shughuli zetu nyingine na si kuruka hewani hadi kwenye dari ili kuweza kutoka vyumbani mwetu kwa shughuli zetu za kawaida.
Tumejifunza hili tangu tukiwa wadogo kabisa na sasa hatuna haja hata ya kufikiria kila siku kwamba hivyo ndivyo tunavyotakiwa kufanya. Vivyo hivyo, pia hatuna haja ya kufikiria ni kwa kiasi gani nguvu ya uvutano ina mchango gani katika kusimama kwetu kila asubuhi tangu tunapoamka vitandani mwetu.
Wakati unapofungua mlango wa nyumba yako, unageuza ufunguo wako kuelekea upande uliko ubao wa kufungia mlango ama upande wa tofauti na mwenendo wa mikono ya saa.
Hiyo ni imani tunayojijengea tangu tukiwa watoto wadogo kabisa, tunapoanza kujifunza kufungua na kufunga milango.
Kila unapokutana na mlango mpya hatuwi na wasiwasi kwamba tunajua vile mlango unavyofunguka kwani tunakuwa na hakika (akilini mwetu) na namna mlango huo utakavyofunguka. Tunazunguusha funguo kuelekea upande uliko mlango tu! Ni rahisi. Hiyo ndiyo imani tuliyonayo.
Huoni sababu ya kufikiria uwezekano wa kukutana na mlango unaofunguka vinginevyo. Lakini hakuna atakayekataa kwamba wengi tumewahi kukutana na milango inayofunguka kwa mwelekeo tofauti na ule tunaoamini ndio utaratibu ‘unaokubalika.’ Inaudhi sana unapokutana nao kwa mara ya kwanza.
Hata baada ya mwaka mzima wa kufungua mlango kwa mwelekeo huo, bado imani uliyojijengea kutokana na uzoefu wako kwamba mlango haufunguki kwa mwelekeo huo, utakuwa nayo, na hivyo utakuwa ukikasirika kila mara utakapofungua mlango huo. Imani unayojijengea moja kwa moja huathiri tabia yako, hata kama imani hiyo si sahihi kama unavyofikiria.
Hebu tufikirie kitu kingine! Dunia ni duara ama si duara? Umelijuaje hili? Si kwamba umeambiwa na watu tu? Una uhakika gani? Wapo wanaoamini kwamba dunia ni ya ubapa kutokana na wanavyoiona kila wanapochungulia madirishani.
Kama ungeamini kwamba dunia ni ya ubapa, ni wazi ungepatwa na wasiwasi mkubwa wakati unaposafiri kwenye mashua kwamba huenda mngefika mwisho na kuangukia nje ya dunia.
Lakini hivi ndivyo watu walivyokuwa wakifikiria. Kilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa ugunduzi kwa miaka mingi ya mwanzoni. Imani waliyokuwa nayo watu moja kwa moja iliathiri vitendo vyao, na hilo lilikwaza matokeo yao.
Fahamu tena kwamba imani si lazima zioneshe ukweli uliopo duniani. Si kila siku milango hufunguliwa kuelekea mwelekeo uliko mlango.
Imani kuhusu dunia kuwa ubapa ilibadilishwa mara wagunduzi walipoanza kuzunguuka dunia. Imani huathiri moja kwa moja matendo yetu hata hivyo. Wakati mwingine, tunachukua hatua hata imani zetu zinapokuwa si sahihi, na hii yaweza kutukwaza. Hii ni kweli kuhusiana na imani tulizonazo kuhusu nafsi zetu na uwezo wetu.
Vipi kuhusu nafsi zetu? Kama tufanyavyo mambo tuliyoyazoea bila kufikiria kutokana na imani tunazojijengea kama vile kufungua mlango, tunafanya hivyo hivyo kutokana na imani tunazojijengea kuhusu nafsi zetu.
Ikiwa tutajenga imani za kutukwaza kuhusiana na nini kinawezekana kufanikisha, jibu letu litakuwa kukwamisha matokeo ya vitendo vyetu tunavyochukua. Matokeo yake tunakwaza pia matokeo tunayoyapata.
Ikiwa tunaamini kwamba kuna kila uwezekano wa kushindwa katika kile tunachofanya mawazo yetu ya kina (subconscious mind), itafanya kazi ya kujenga mazingira yatakayounga mkono imani yetu hii. Wakati mambo yanapokuwa magumu, hatutakuwa na haja ya kufanya jitihada zaidi iliyo muhimu katika kufanikiwa; kushindwa kwa mara ya kwanza kutaunga mkono imani yetu hiyo na hivyo kutufanya tukate tamaa na kuachana na kile tunachofanya.
Kwa upande mwingine, ikiwa tutaamini kwamba tutafaulu, ni lazima tutafaulu. Mohamed Ali aliyekuwa akifahamika kama mwanamichezo aliyefanikiwa kushinda wote waliowahi kutokea duniani, mbali ya ari aliyokuwa nayo, kipaji na nguvu zake, moja ya sababu kuu zilizomsadia kufanikiwa na kuwa maarufu kiasi alichokuwa ni kwamba alikuwa na imani nzito kuhusiana na kila alichotaka kufanya.
Wengi tumewahi kuona picha zake za televisheni wakati akiwa ulingoni, alipokuwa akidai kwamba yeye ndiye bondia bora kushinda wote waliowahi kutokea duniani. Wakati alipokuwa akiieleza dunia hivi, ni kweli alikuwa bondia bora kushinda wote duniani? Wakati ule hakuwa hivyo, kwani alikuwa bado ana mambo ya kuionesha dunia ili kuthibitisha hilo. Alichokuwa nacho hata hivyo ni kujiamini moja kwa moja katika uwezo wake. Imani hiyo ilithibitishwa na matokeo aliyoyapata licha ya kuvuliwa mkanda wake wa dunia mwaka 1967, baada ya kukataa kwenda kupigana vita Vietnam akiwa askari wa jeshi la Marekani, hakukata tamaa.
Alirudi tena miaka saba baadaye na kushinda ubingwa huo alioendelea kukaa nao kwa miaka minne zaidi. Imani yake kwamba yeye ndiye bora kuliko wote waliowahi kutokea duniani, si kwamba ilimsaidia kufikia kiwango cha juu cha masumbwi, bali kiwango cha juu cha michezo kwa ujumla